AhlulBayt News Agency

source : Alumni.miu.ac.ir
Wednesday

23 December 2015

1:15:57 PM
726471

Full Text;

Second Message of Ayatollah Khamenei to the Western Youth in Swahili

Second Message of Ayatollah Khamenei to the Western Youth in Swahili.

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaandikia barua (ya pili) vijana wote wa nchi za Magharibi na kuyataja matukio ya kigaidi yaliyotokea nchini Ufaransa hivi karibuni kuwa yanaandaa uwanja wa kuwepo fikra za pamoja na huku akitoa mifano kadhaa inayoumiza nyoyo inayotokana na ugaidi unaofanyika katika ulimwengu wa Kiislamu kwa uungaji mkono wa baadhi ya madola makubwa, kuungwa mkono ugaidi wa kiserikali unaofanywa na Israel na kutumwa majeshi ya kigeni yaliyosababisha hasara kubwa katika miaka ya hivi karibuni kwenye ulimwengu wa Kiislamu, amezungumza na vijana na kuwasisitizia kwa kuwaambia: Ninakutakeni vijana muweke misingi ya muamala sahihi na wa heshima kuhusiana na ulimwengu wa Kiislamu kwa kutegemea welewa sahihi na wa kina na kwa kutumia uzoefu wa matukio machungu. Matini kamili ya barua hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim
Kwa vijana wote wa nchi za Magharibi

Matukio machungu ambayo yamesababishwa na ugaidi kipofu nchini Ufaransa kwa mara nyingine yamenifanya tuzungumze na nyinyi vijana. Kwa kweli ninasikitika kuona kuwa matukio kama haya yanakuwa msingi wa mazungumzo yangu lakini ukweli wa mambo ni kuwa, iwapo masuala machungu hayatachukuliwa kuwa msingi wa kufikiriwa njia za utatuzi na kuwa chombo cha fikra za pamoja, bila ya shaka hasara ya masuala hayo itakuwa maradufu. Machungu ya kila mwanadamu katika kila pembe ya dunia huwatia huzuni wanadamu wenzake. Mandhari ya mtoto anayekata roho mbele ya wapendwa wake, mama ambaye furaha ya familia yake hubadilika na kuwa maombolezo, mume ambaye hubeba mwili usio na roho wa mkewe na kuupeleka harakaharaka sehemu fulani au mtazamaji ambaye hajui kuwa dakika chache zijazo huenda pazia la mwisho la tamthilia ya maisha yake litafungwa, bila ya shaka yoyote ni mandhari ambazo zinaziathiri hisia za kila mwanadamu. Mtu yeyote mwenye hisia za mapenzi na ubinadamu ataathirika na kuumizwa na matukio hayo popote yanapotokea, yawe yanatokea nchini Ufaransa au Palestina au Iraq au Lebanon au Syria. Hapana shaka kuwa Waislamu bilioni moja na nusu wana hisia hiyo hiyo na wanachukizwa na kukerwa na watendaji na wasababishaji wa maafa hayo. Ama suala muhimu hapa ni kwamba, iwapo machungu ya leo hayatapelekea kujengwa kesho iliyo bora na iliyo na amani zaidi, basi yatabakia kuwa kumbukumbu za matukio machungu tu zisizo na faida yoyote. Ninaamini kuwa, ni nyinyi tu vijana ndio mnaoweza kujifunza kutokana na misukosuko ya leo na kuweza kupata njia mpya za kujenga mustakbali na kuzuia upotofu ambao umewafikisha Wamagharibi hapa walipo hivi sasa.

Ni kweli kuwa ugaidi leo hii umekuwa ni machungu ya pamoja kati yetu na nyinyi, lakini ni muhimu mufahamu kuwa, ghasia na wasiwasi ambao umekukumbeni katika matukio ya hivi karibuni, una tofauti mbili kubwa na machungu ambayo yamekuwa yakiwatesa watu wa Iraq, Yemen, Syria na Afghanistan kwa miaka mingi. Tofauti ya kwanza ni kuwa, ulimwengu wa Kiislamu umekuwa mhanga wa unyama, hofu na ghasia kubwa zaidi tena na kwa muda mrefu sana na pili ni kwamba, kwa masikitiko makubwa, ghasia hizo zimekuwa zikichochewa na kuungwa mkono na madola makubwa na kwa njia tofauti na zenye taathira. Hii leo ni watu wachache mno ambao hawana habari kuhusu nafasi ya Marekani katika kuyaanzisha au kuyaimarisha na kuyapa silaha (makundi ya) al Qaida, Taliban na makundi mengine maovu yenye uhusiano na makundi hayo. Mbali na uungaji mkono huo wa moja kwa moja, waungaji mkono wa wazi na wanaojulikana wa utakfiri ambao wana mifumo iliyodumaa mno kisiasa, daima wanahesabiwa kuwa washirika muhimu wa nchi za Magharibi; na hii ni katika hali ambayo fikra bora na zilizo wazi zaidi zinazotokana na demokrasia safi na ya asili kabisa katika eneo (hili la Mashariki ya Kati) zinakandamizwa bila huruma. Miamala ya kindumakuwili ya Magharibi kuhusiana na mwamko kama huu katika ulimwengu wa Kiislamu ni mfano wa wazi wa mgongano uliopo katika siasa za Magharibi.

Mfano mwingine wa mgongano huo unaonekana katika kuunga mkono ugaidi wa kiserikali wa Israel. Ni zaidi ya miaka 60 sasa tokea wananchi madhlumu wa Palestina waanze kusulubiwa kwa aina mbaya zaidi ya ugaidi. Ikiwa watu wa Ulaya kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakijificha kwenye nyumba zao na kuogopa kushiriki kwenye mikusanyiko na vituo vilivyo na umati mkubwa wa watu, ni kwa makumi ya miaka sasa ambapo familia za Kipalestina hazina usalama hata ndani ya nyumba zao kutokana na mauaji na uharibifu ya utawala wa Kizayuni. Leo hii ni utumiaji mabavu upi unaoweza kulinganishwa na unyama wa utawala wa Kizayuni unaotendwa kupitia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni? Utawala huo kila siku hubomoa nyumba za Wapalestina na kuanganiza mabustani na mashamba yao bila ya hata kuwapa fursa ya kuondoa vitu vyao na vyombo vyao wanavyovitumia katika maisha yao ya kila siku na wala mazao yao ya kilimo. (Utawala wa Kizayuni unafanya jinai hizo) bila ya kukosolewa au kukemewa na washirika wake walio na ushawishi mkubwa au kwa uchache taasisi za kimataifa ambazo kidhahiri zinaonekana ni huru. Aghlabu unyama huo hufanyika mbele ya macho yanayobubujika machozi ya watoto na wanawake waliojawa na hofu kubwa ambao hushuhudia jamaa zao wakipigwa na kujeruhiwa na mara nyingine kupelekwa kwenye jela za kuogofya na za mateso (za Wazayuni). Je, mnajua ukatili mwingine mkubwa zaidi ya huu katika zama hizi na wa muda mrefu kama hivi katika sehemu nyingine yoyote ya dunia ya leo? Kama kuuliwa kwa risasi mwanamke barabarani kwa sababu tu ya kumlalamikia askari aliyejizatiti vilivyo kwa silaha, si ugaidi ni nini? Je, kwa kuwa ukatili huu unafanywa na wanajeshi wa utawala vamizi haupasi kuitwa kuwa ni misimamo ya kuchupa mipaka? Au kwa vile picha hizi zimekuwa zikionyeshwa na kukaririwa kwenye televisheni kwa miaka 60, hazina nguvu tena za kuchochea hisia zetu?

Kumiminwa majeshi (ya madola ya kigeni) katika miaka ya hivi karibuni kwenye nchi za ulimwengu wa Kiislamu kitendo ambacho tayari kimeshachukua wahanga wengi, ni mfano mwingine wa mantiki inayogongana ya Magharibi. Nchi zinazohujumiwa mbali na kupata hasara za kibindamu, zimepoteza pia miundombinu yao ya kiuchumi na kiviwanda, harakati zao za maendeleo na ustawi zimesimama au kupungua kasi na hata katika baadhi ya sehemu zimerejea nyuma kwa makumi ya miaka. Licha ya hayo na kwa kiburi, nchi hizo zinatakiwa zisijihesabu kuwa ni nchi zinazodhulumiwa. Inawezekana vipi nchi ambazo zimeharibiwa kwa kiwango hiki na miji na vijiji vyao vimefanywa jivu zinaambiwa: Tafadhali msijihesabu kuwa mliodhulumiwa?! Je, si bora kuomba msamaha kwa udhati wa moyo badala ya kujitia kutoelewa au kujifanya maafa yaliyotendwa? Mateso ya kiroho ambayo yameupata ulimwengu wa Kiislamu katika miaka ya hivi karibuni kutoka kwa wahujumu walio na nyuso mbili zilizorembwa nayo si madogo ikilinganishwa na hasara ya kimaada.

Vijana wapenzi! Ninatumai kuwa nyinyi hivi sasa au katika siku zijazo mtaweza kubadilisha mtazamo na fikra hii potofu, fikra ambayo kipaji chake wake ni kuficha malengo ya muda mrefu na kupamba malengo ya kuudhi. Kwa mtazamo wangu hatua ya kwanza ya kuleta usalama na utulivu, ni kurekebisha fikra hii ya kutumia mabavu. Maadamu vipimo vya kindumakuwili vitaendelea kudhibiti na kughilibu siasa za Magharibi; madhali kugawanywa ugaidi na waungaji mkono wake wenye nguvu katika makundi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya kutaendelea, na maadamu maslahi ya serikali yataendelea kufadhilishwa na kuwekwa mbele ya thamani za kiutu na maadili, tujue kuwa mizizi ya utumiaji mabavu haipaswi kutafutwa kwingine ghairi ya ndani ya mambo hayo.

Inasikitisha sana kuona kuwa mizizi hii, imejikita pia hatua kwa hatua kwa miaka mingi katika sera za kiutamaduni za Magharibi na kuandaa mazingira ya kujitokeza hujuma laini na ya kimya kimya.
Nchi nyingi za dunia zinajivunia utamaduni wao wa jadi na wa kitaifa; hizi ni tamaduni ambazo sambamba na kuinuka na kustawi, zimekuwa zikikidhi vyema mahitaji ya jamii za mwanadamu kwa mamia ya miaka. Ulimwengu wa Kiislamu nao pia hauko nje ya duara hili. Lakini katika zama zetu hizi, ulimwengu wa Magharibi unatumia suhula za kisasa ili kulazimisha kuwepo utamaduni unaoshabihiana na unaofanana kote duniani. Mimi ninaamini kuwa, kujaribu kuyatwisha mataifa mengine utamaduni wa Magharibi na kuziona duni tamaduni huru ni utumiaji mabavu wa kimya kimya na wenye madhara makubwa sana.

Mwenendo huu wa kudhalilisha tamaduni tajiri na kuvunjia heshima matukufu makubwa zaidi ya tamaduni hizo unafanyika katika hali ambayo, tamaduni mbadala hazina sifa na uwezo wa kuchukua nafasi ya tamaduni hizo. Kwa mfano, mambo mawili ya "ushari" na "ufuska na utovu wa maadili" ambayo, kwa masikitikio, yamekuwa misingi mikuu ya utamaduni wa Magharibi, yamepoteza nafasi hata huko huko yalikozaliwa. Hapa swali linalojitokeza ni kwamba, je, tutakuwa watenda dhambi na makosa iwapo tutaukataa utamaduni wenye kupenda machafuko, wa ufuska na usiokubali masuala ya kiroho? Je, tutakuwa tunakosea iwapo tutazuia mafuriko na uharibifu ambao unakuja kwa vijana wetu katika kalibu ya bidhaa za kisanaa? Mimi sipingi umuhimu na thamani za mahusiano ya kiutamaduni. Mahusiano hayo yanapofanyika katika mazingira ya kawaida na kwa kuheshimu jamii husika huitunuku jamii hiyo ustawi, maendeleo na huitajirisha. Mkabala wake, mahusiano yasiyooana na ya kulazimishwa hufeli na husababisha hasara. Kwa masikitiko nalazimika kusema kwamba, makundi maovu kama Daesh ni wazaliwa na ni matokeo ya maingiliano kama hayo yasiyo na mafanikio na tamaduni kutoka nje. Kama kweli tatizo lingekuwa ni la kiitikadi basi tatizo hili pia lingelishuhudiwa katika ulimwengu wa Kiislamu kabla ya zama za ukoloni, hata hivyo historia inathibitisha kinyume chake. Nyaraka za kuaminika za kihistoria zinaonesha waziwazi jinsi muungano wa ukoloni na fikra za kuchupa mipaka na zisizokubalika, tena ndani ya kabila moja la kibedui, ulivyopandikiza mbegu ya misimamo mikali katika eneo hili. La sivyo inawezekana vipi kutokea taka kama Daesh katika moja ya mifumo ya kidini (Uislamu) wenye maadili bora zaidi na ya kibinadamu zaidi duniani ambao unasisitiza katika misingi na nguzo zake kwamba kutoa roho ya mwanadamu mmoja ni sawa na kuua wanadamu wote?

Katika upande mwingine inatupasa kuuliza kwamba, ni kwa nini watu waliozaliwa Ulaya na kupata malezi ya kifikra na kiroho katika mazingira hayo wakavutwa na kuathiriwa na makundi hayo (ya kigaidi na kitakfiri)? Je, inawezekana kuamini kwamba, watu hawa ghafla moja wameweza kuwa na misimamo ya kuchupa mipaka kwa kutembelea mara moja au mbili maeneo ya vita kiasi cha kuwafanya wawamiminie risasi wananchi wenzao? Bila ya shaka (katika mazingira kama haya) haiwezekani kusahau na kupuuza taathira za kipindi kirefu cha kulishwa utamaduni usio sahihi katika mazingira machafu na yanayozalisha ukatili (ya nchi za Magharibi). Tunapaswa kuwa na uchambuzi kamili na wa pande zote, uchambuzi utakaobaini uchafu wa dhahiri na wa batini wa jamii. Inawezekana kwamba chuki kubwa iliyopandikizwa katika nyoyo za matabaka mbalimbali ya jamii za Magharibi kwa kipindi cha miaka mingi ya ustawi wa kiviwanda na kiuchumi na kutokana na dhulma na wakati mwingine ubaguzi wa kisheria na kimuundo, imezusha vinyongo ambavyo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara kama maradhi katika sura hii.

Alaa kulli hal, sasa mnalazimika kuvunja tando za kidhahiri za jamii zenu, mupate kuondoa vifundo na vinyongo vilivyomo. Nyufa zilizopo zinapaswa kurekebishwa badala ya kupanuliwa zaidi. Kosa kubwa katika kupambana na ugaidi ni kuchukua misimamo ya kukurupuka itakayozidisha mipasuko iliyopo. Harakati yoyote ya kijazba na ya kukurupuka ambayo itaitenga au kuitia hofu na kuiweka katika misukosuko jamii ya Waislamu wa Ulaya na Marekani ambayo ina mamilioni ya watu wenye kujituma na kuwajibika, na ikapelekea kunyimwa zaidi haki zao za kimsingi na kuwaweka kando, si tu haitatatua tatizo, bali hata itapanua zaidi nyufa na kuzidisha vinyongo. Hatua za kijuujuu na misimamo ya kukurupuka hususan pale inapohalalishwa kisheria, mbali na kwamba haitakuwa na matokeo ghairi ya kuzidisha kambi zilizopo, vile vile itafungua njia ya kuzuka migogoro mipya katika siku za usoni.

Habari zilizotufikia zinasema kuwa, katika baadhi ya nchi za Ulaya kumewekwa taratibu zinazowalazimisha raia kufanya ujasusi dhidi ya Waislamu. Mwenendo huu ni wa kidhalimu na sisi sote tunajua kwamba - kwa kupenda au bila ya kupenda - dhulma ina sifa ya mwangwi. Zaidi ni kwamba Waislamu hawastahiki kufanyiwa utovu huo wa fadhila. Dunia ya Magharibi inawajua vyema Waislamu kwa karne nyingi. Wakati Wamagharibi walipokuwa wageni katika ardhi ya nchi za Kiislamu na kukodolea macho utajiri wa mwenye nyumba, na vilevile wakati mwingine ambapo walikuwa wenyeji na wakafaidika na kazi na fikra za Waislamu, aghlabu hawakuona lololote kutoka (kwa Waislamu) isipokuwa ukarimu na uvumilivu.
Kwa msingi huo ninawataka nyinyi vijana, mjenge nguzo za kuamiliana kwa njia sahihi na kiungwana na ulimwengu wa Kiislamu kwa msingi wa utambuzi sahihi, muono mpana na kwa kutumia tajiriba chungu. Iwapo mtafanya hivyo mutaona katika kipindi si kirefu kijacho, jengo mlilojenga juu ya nguzo hizo imara linaweka kivuli cha imani na kuaminiana juu ya vichwa vya wahandisi wa jengo hilo na kuwatunuku vuguvugu la amani na utulivu na hatimaye kumulika mwanga wa matumaini katika mustakbali wa dunia.

Sayyid Ali Khamenei
8/Azar/1394
(29/Novemba/2015 ).